Ngeli
Ngeli ni makundi ya kisarufi ya majina katika lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za Kibantu.
Kwa maneno mengine, ngeli za nomino ni utaratibu unaotumika kuweka nomino katika matabaka au makundi yanayofanana.
- Mifano
- Maji yakimwagika hayazoleki.
- Mayai yaliyooza yananuka sana.
- Yai lililooza linanuka sana.
- Maji lililomwagika hayazoleki.
Katika mifano hiyo juu tunaona kwamba sentensi a, b na c ziko sahihi wakati sentensi d si sahihi, kwa sababu imekiuka upatanisho wa kisarufi. Kwa maana hiyo sentensi ‘a’ ipo katika ngeli ya YA-YA na sentensi b na c zipo katika ngeli ya LI-YA. Sentensi si sahihi kwa sababu nomino maji haina umoja, kwa hiyo haiwezi kuingia katika ngeli ya LI-YA. Kwa msingi huo ngeli za nomino huzingatia sana upatanisho wa kisarufi.
Kwa ujumla, ngeli za Kiswahili huainishwa kulingana na viambishi mbalimbali ambavyo nomino tofauti huchukua katika umoja na wingi.
Mipangilio na idadi yake
haririJedwali lifuatalo linaonesha ngeli za nomino kwa misingi ya upatanisho wa kisarufi.
Ngeli | Ufafanuzi | Mifano |
---|---|---|
A-WA | Ngeli hii inahusisha majina ya viumbe hai kama vile watu, wanyama, ndege, wadudu n.k | Sungura mjanja ameumia
Sungura wajanja wameumia Mkuu anawasili |
LI-YA | Majina yenye kiambishi awali li- katika umoja na ya- katika wingi huingia katika ngeli hii | Jambia la babu limepotea
Majambia ya babu yamepatikana |
KI-VI | Ni ngeli ya majina ya vitu visivyo hai, yanayoanza kwa KI- au CH- (umoja); na VI- au VY- (wingi). Pia ngeli hii hujumuisha majina ya vitu vingine katika hali ya udogo k.v, kijito, kilima | Chakula kimekwisha
Vyakula vimekwisha Kijito kimekauka Vijito vimekauka |
U-I | Huwakilisha majina ya vitu visivyo hai, yaanzayo kwa sauti M- (umoja) na MI- (wingi). Pia majina ya baadhi ya viungo vya mwili huingia humu, kwa mfano mkono, mguu, mkia n.k | Mlima umeporomoka
Milima imeporomoka Mkono umevunjika Mikono imevunjika Mito hii ina mamba wengi |
U-ZI | Hurejelea majina ambayo huanza kwa U- (umoja) na huchukua ZI- kama kiambishi kiwakilishi cha ngeli katika wingi. Majina yenye silabi tatu au zaidi hubadilishwa kwa wingi kwa kutoa sauti /u/' k.v ukuta-kuta. Majina ya silabi mbili huongezewa /ny/ katika wingi. k.v ufa - nyufa | Ukuta umebomoka
Kuta zimebomoka Wimbo huu unavutia Nyimbo hizi zinavutia Ufa umeonekana Nyufa zimeonekana |
I-ZI | Hutumiwa kwa majina yasiyobadilika kwa umoja wala kwa wingi lakini huchukua viambishi viwakilishi tofauti: I- (umoja) na ZI- (Wingi). | Nyumba imejengwa
Nyumba zimejengwa Salam imefika Salam zimefika |
U-YA | Ngeli hii inajumuisha nomino ambazo zina kiambishi awali u- katika umoja na ma- katika wingi. | Ukuu umekuponza
Makuu yamekuponza Unyoya unapepea Manyoya yanapepea |
KU | Majina yanayotokana na vitenzi yanayoanza na ku- (vitenzi-jina) | Kusoma kwako kumekusaidia
Kuchelewa kumemponza |
PA/MU/KU- | Huonyesha mahali | Amekaa pale palipo na wadudu wengi
Amelala mule mulimojaa siafu. Amepita kule mbali |
Matumizi ya ngeli
haririHapa tunaona dhima ya matumizi yake.
- Hutumika kupanga majina ya lugha katika makundi yaliyoshikamana na kutofungamana kutokana na kigezo muhimu.
- Hutumika kutambulisha maumbo ya umoja na wingi katika majina na vivumishi.
- Hutumika katika upatanishi wa kisarufi katika sentensi.
- Hutumika katika kuonyesha uhusiano uliopo baina ya lugha za Kiswahili na lugha nyingine.
Dhana ya O-rejeshi
haririO-rejeshi ni kiambishi kinachotumiwa kurejelea nomino ambayo huwa imetajwa kabla ya kitenzi chenyewe kutajwa. Viambishi hivyo ndivyo vinavyosababisha utegemezi katika sentensi.
Dhima kuu ya muundo wa O-rejeshi
haririHutumika kama kirejeshi. Kwa mfano:
- Mtu aliyepigwa jana na wananchi ni mfanyabiashara wa Mwanza.
- O-rejeshi hudokeza mahali. Kwa mfano; rudisha ulipokitoa!
- O- rejeshi hudokeza wakati. Kwa mfano; Alipokuja alinikuta nimelala.
- Vilevile hutumika kama kiunganishi. Kwa mfano; Alikuja. Nilikuwa nimelala (alipokuja alinikuta nimelala)
- Hudokeza namna. Mfano; Kila mtu anashangaa alivyoumia.
Kwa jumla, ngeli za Kiswahili huainishwa kulingana na viambishi mbalimbali ambavyo nomino tofauti huchukua katika umoja na wingi.