Location via proxy:   [ UP ]  
[Report a bug]   [Manage cookies]                

Njia ya Jua (kwa Kiingereza: ecliptic) ni mstari wa kudhaniwa kwenye anga la Dunia ambako Jua linapita mbele ya nyota katika muda wa mwaka mmoja.

Kwa mtazamaji kwenye Dunia yetu, Jua linabadili mahali pake kulingana na nyota zinazoonekana nyuma yake. Hilo linaonekana vema kwa kulinganisha nyota zinapoonekana kwenye sehemu ya mapambazuko au machweo ya Jua angani katika mwendo wa mwaka. Baada ya siku 365 mwendo huu unarudia. Hali halisi ni Dunia inayozunguka Jua na hivyo tunaona nyota tofauti-tofauti „nyuma“ ya Jua.

Asili ya kutambua njia ya Jua

Njia ya Jua haionekani kirahisi kwa macho kwa sababu tunaona Jua wakati wa mchana ambako nyota hazionekani.

Lakini wakati wa mapambazuko na machweo nyota zinaanza kuonekana tukiweza kutambua ni karibu na nyota gani ya kwamba jua linapambazuka na kuchwa.

Tukiangalia tena nyota zilizopo angani karibu na sehemu ya kuchwa baada ya wiki 4 tunaona kumbe zimekuwa tofauti. Nyota hizi katika sehemu ambako Jua linatokea au kupotea kwa macho ya mtazamaji zinabadilika mwezi kwa mwezi lakini baada ya mwaka mmoja ni tena nyota zilezile.

Zodiaki au mzingo wa mwaka

Tangu miaka elfu kadhaa watazamaji wa nyota katika tamaduni mbalimbali za Dunia walishika kumbukumbu ya mabadiliko hayo yanayotokea sambamba na mabadiliko ya majira.

Vilevile tangu kale watu waliwahi kupanga nyota za angani katika kundinyota. Kwa jumla ni makundinyota 12 ya kurudia zilizoonekana tangu kale ya kuwa Jua linapita katika maeneo yake katika muda wa mwaka. Mzingo unaounganisha makundinyota haya 12 ambako Jua linapita ni mstari wa njia ya Jua.

Jina "ecliptic" linatokana na neno la Kigiriki Εκλειψις ekleipsis linalotaja Kupatwa kwa Jua au Kupatwa kwa Mwezi. Maana kila mara tukio kama hili linatazamwa Jua au Mwezi uko kwenye mstari wa njiajua.

Makundinyota karibu yote kwenye mstari wa njia ya Jua yanataja wanyama wa mitholojia ya Kigiriki. Wagiriki wa Kale wakiona hasa sura za wanyama fulani katika mstari huu wakaita mzingo wote ζῳδιακὸς κύκλος zoodiakos kiklos, yaani "mzingo wa wanyama". Hapa ni asili ya jina la Zodiaki (pia Zodiki) linalotumiwa katika lugha nyingi.

Waarabu wanasema hapa دائرة البروج dairat-al-buruj "mzingo wa minara" kwa sababu wanaita makundinyota haya "minara za falaki" na dhana hili lilipokewa katika Kiswahili kwa jina la "buruji za falaki".

Miendo ya Jua inayoonekana

Hali halisi Jua linakaa katika kitovu cha mfumo wa Jua likizungukwa na sayari, na wakati huohuo unazunguka polepole kitovu cha Njia Nyeupe pamoja na mfumo wake wa sayari, miezi na asteroidi.

Dunia yetu ni sayari mojawapo inayozunguka kwenye mhimili wake ukifuata obiti yake ya kuzunguka Jua. Lakini hii hatuwezi kuona moja kwa moja na hali hii imetambuliwa tu wakati wa karne iliyopita.

Kwa macho ya mtazamaji aliye duniani kuna miendo miwili tofauti ya Jua:

* Mwendo wa Jua kuhusiana na Dunia: Jua linapita angani kuanzia mashariki hadi magharibi, kila siku likipita kilele cha anga wakati wa mchana. Vilevile nyota zinaonekana zinazunguka angani sawa na Jua lakini wakati wa usiku. Asubuhi inayofuata Jua linatokea tena palepale, au karibu palepale ilipoonekana siku ya jana.

* Mwendo wa Jua kuhusiana na Nyota: Mwendo wa pili ni ule wa jua mbele ya nyota ambao linaonekana kufuata mzingo wa kila mwaka yaani Zodiaki.

 
Bapa la mfumo wa Jua tunapokuta obiti zote za sayari.

Bapa la Mfumo wa Jua

Msingi wa kutambua njia ya Jua ni umbo la Mfumo wa Jua letu. Leo hii inadhaniwa asili yake ni mzunguko wa masi kubwa wa vumbi iliyokuwa takriban na umbo la sahani iliyozunguka.

Sehemu kubwa ya masi ilijikaza katika kitovu na kuwa Jua lenyewe. Katika sehemu za nje ya sahani hiyo palikuwa na sehemu mbalimbali ambako masi ilijikaza pia; masi hizi hazikutosha kuanzisha mchakato wa kinyuklia hivyo ni vyanzo vya sayari.

Katika sehemu nyingine masi hazikutosha kujikaza na hapo tunapata sehemu za Mfumo wa Jua kama vile ukanda wa asteroidi kati ya Mirihi na Mshtarii au ukanda wa Kuiper ng'ambo ya sayari Neptun.

Kutokana na asili ya pamoja katika sahani asilia ya mfumo wa Jua tunakuta sayari zote zinapatikana takriban katika bapa moja. Pia miendo yote ya sayari inafuata mwelekeo huohuo.

Kwa hiyo bapa hilo huitwa pia "bapa la njia ya Jua" .