Siku
Siku ni muda wa saa 24 ambamo tunaona vipindi viwili: kile cha mwanga wa mchana na kile cha giza la usiku.
Mchana na usiku
Mabadiliko hayo ya mchana na usiku husabibishwa na mzunguko wa dunia kwenye mhimili wake. Upande wa dunia unaotazama jua unapata mwanga wa mchana lakini upande mwingine usiotazama jua unakuwa gizani.
Sisi pamoja na vitu vyote vilivyo juu ya uso wa dunia, yaani bahari, mito, milima, binadamu, misitu, majangwa, majengo, barabara na kila kitu unachoweza kuwaza kuwa kipo kwenye uso wa dunia, basi vyote huwa katika mwendo kadiri dunia inavyojizungusha kwenye mhimili wake. Hivyo basi, wakati upande ule wa uso wa dunia tulipo unapogeukia au kutazamana na jua, basi kwetu inakuwa mchana, pale ambapo upande huo hatutazamani na dunia, basi tunapata usiku, yaani tunakuwa kwenye giza.
Mwanzo na mwisho
Mwanzo na mwisho wa siku ni jambo la mapatano baina ya watu ma hapa kuna kawaida tofautitofauti katika tamaduni za Dunia.
Uchumi na sheria siku hizi hufuata muda sanifu wa dunia unaopanga mwisho na mwanzo wa siku ya kalenda katikati ya usiku, yaani saa sita usiku, au kwa lugha nyingine kwenye 24:00 au 0:00 h.
Kalenda za kidini kama kalenda ya Kiyahudi na Kalenda ya kiislamu hupanga mwisho wa siku wakati wa machweo, ambayo ni pia mwanzo wa siku mpya. Kwa sababu hiyo sherehe ya Sabato katika Uyahudi (ambayo inalingana na Jumamosi ya Kiswahili) inaanza baada ya machweo kwenye Ijumaa, na pia utaratibu wa kuzuia kazi unakwisha kwenye jioni ya Jumamosi baada ya machweo.
Muda wa siku
Mzunguko huo wa dunia kwenye mhimili wake unachukua muda wa nukta (sekunde) 86,400 au masaa 24.
Kwa sababu muda wa mzunguko haulingani kikamilifu na kipimo cha sekunde kuna siku ndefu au fupi zinazopatikana kwa kuingiza au kupunguza nukta moja kufuatana na azimio ya wataalamu wa wakati. Hii haina umuhimu wowote katika maisha ya kila siku lakini inapaswa kuangaliwa pale ambapo saa kamili sana ya kiatomi hutumiwa.
Siku na mwaka
Dunia, pamoja na kujizungusha kwenye mhimili wake, ina mwendo mwingine pia , yaani ule wa kulizunguka jua. Ikikamilisha mwendo huu basi mwaka unakuwa umekamilika. Kipindi cha mwaka hakilingani kwa kila mwaka: kuna miaka mirefu na miaka mifupi. Hii ni kwa mujibu wa Kalenda ya Gregori ambapo mwaka wa kawaida (mfupi) huwa na siku 365 na kila mwaka wa nne (mwaka mrefu) kuwa na siku 366.