Jicho
Jicho ni sehemu ya mwili inayowezesha kuona. Ni ogani inayotambua mwanga na kutuma habari zake kwa ubongo.
Aina za macho ya viumbehai
Kuna mifumo mbalimbali ya macho kati ya aina mbalimbali za wanyama.
Macho ya kimsingi kwa viumbehai vidogo yanatambua tu kama mazingira yana mwanga au la. Hata kati ya viumbehai wenye seli moja kuna wenye protini zinazotofautisha giza na nuru. Kuna konokono ambao hawawezi "kuona" picha ya mazingira lakini wanatambua mwanga na uwezo huu unawawezesha kuepukana na mwanga wa jua ambao ungewakausha.
Macho yaliyoendelea kiasi yana umbo kama kikombe na hili linawezesha kutambua upande gani nuru inatokea.
Wanyama wengi huwa na macho yaliyoendelea zaidi: yana uwezo wa kuona picha halisi ya mazingira pamoja na rangi na mwendo.
Macho ya kuungwa
Wadudu na arthropoda huwa na macho ya kuungwa na vijicho vingi vidogo vinavyoitwa omatidi; kila kijicho huwa na umbo la kijiti na kwenye mwisho wake kuna lenzi ya chitini. Mdudu anaweza kuwa na vijicho elfu kadhaa na picha ya mazingira inaunganishwa kutokana na picha nyingi ndogo za kila kijicho.
Macho haya ya kuungwa yanamwezesha mdudu kuangalia asilimia kubwa ya mazingira yake: kwa aina kadhaa hata nyuma yake. Macho ya kuungwa yanaweza kufunika hadi asilimia 80 ya eneo la kichwa. Mdudu haoni vikali kama mtu lakini anaona mabadiliko na mwendo haraka sana.
Wanyama wanaoishi katika vilindi vya bahari penye giza nene huwa na macho ambamo fuwele ziko kama kioo na kupazia nuru hafifu.
Kuna wanyama wanaoweza kuona nuru ambayo ni nje ya upeo wa kibinadamu; kwa mfano nyuki huona mnururisho wa infraredi.
Macho ya mamalia
Macho ya binadamu kama ya mamalia wengine huwa na lenzi moja tu. Lakini muundo wa jicho unaruhusu kuona rangi, umbali na mengi madogo.
Shida za macho
Shida za macho ni nyingi kama vile upofu, kutoona rangi, macho kujiliza, wekundu uliokithiri pamoja na kutoa majimaji. Shida hizo huletwa na vumbi, kuzaliwa ukiwa kipofu, jua jingi bila kuvalia miwani vizuia jua.
Viungo vya nje
- http://www.bausch.com/your-eye-concerns/diseases-and-disorders Ilihifadhiwa 22 Februari 2018 kwenye Wayback Machine.
Makala hii kuhusu mambo ya anatomia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Jicho kama matumizi yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |