Nikotini
Nikotini ni dutu ya alkaloidi katika mimea mbalimbali (hasa mtumbaku) ambayo ni dawa linaloathiri neva za mwanadamu. Matumizi yake ni hasa katika sigara, lakini pia katika kemikali na madawa.
Kuanzia kiasi fulani ni sumu kali, kwa viwango vidogo inaamsha neva za watu. Hatari yake kwa mwanadamu ni hasa uzoefu unaotokea na kugeuka haraka uraibu unaotawala mwili na akili kwa hamu ya kurudia matumizi ya nikotini. Katika sifa hii inafanana na madawa ya kulevya hata kama kiwango cha kumwamsha mtu haufikii hali ya ulevi wa namna yoyote.
Jina
haririJina la dawa linatokana na jina la kitaalamu la mtumbaku "Nicotiana tabacum" na hili lilitokana na Jean Nicot de Villemain aliyekuwa balozi wa Ufaransa nchini Ureno katika karne ya 16. Alijipatia mbegu za mtumbaku wakati mmea huu ulikuwa umeingia Ulaya kutoka Amerika akazituma Paris kwa utafiti. Ndiye mtu wa kwanza kuleta mbegu ya mtumbaku nchini Ufaransa.
Dawa ya nikotini ndani ya majani ya mmea liligunduliwa na wanakemia Wajerumani mwaka 1828.
Matokeo ya nikotini yanayotafutwa na watu
haririMatokeo ya kimwili ya nikotini kwa kiwango kidogo ni kuharakisha pigo la moyo na kupandisha kanieneo ya damu. Sifa hii inatafutwa na watu wakisema matumizi ya tumbaku husaidia kuondoa au kupunguza uchovu na kuamsha ubongo. Lakini uamsho huu haudumu muda mrefu na mtu anapaswa kuongeza nikotini mara nyingi kwa kuvuta sigara nyingine.
Hasara na hatari zake
haririHatari hasa ya dawa lenyewe ni uraibu wa hatari ya kutawaliwa nayo.
Sumu ya neva
haririKwa viwango kikubwa zaidi hatari zake kama sumu ya neva ni muhimu. Kiwango cha miligramu moja ya nikotini kwa kilogramu moja ya uzani wa mtu kinatosha kumwua mtu. Yaani mtu mwenye uzani wa kg 70 hufariki akiingiza miligramu 70 mwilini. Hapa ni kwa mfano hatari ya watoto wadogo kula sigara bila kujijua: sigara moja huwa na miligramu 10 za nikotini. Mvutaji anaingiza sehemu yake tu kwa njia ya moshi lakini mlaji anapata yote na mtu mdogo huwa hatarini kabisa.
Nikotini ni kati ya sumu kali kabisa, hivyo imetumiwa kama dawa la wadudu kwa sababu mimea haina matatizo nayo, ni wanyama tu. Lakini nchi nyingi zimepiga marufuku matumizi haya kutokana na hatari kwa watu wanaotumia dawa au wanaoishi katika mazingira ambako inatumiwa.
Sumu katika moshi wa sigara
haririHasara za nikotini katika sigara zinaenda sambamba na kemikali zinazokuja pamoja nayo katika sigara kama njia kuu ya kutumia nikotini. Hapa wataalamu hawana uhakika kiasi gani magonjwa yanayoonekana kati ya wavutaji husababishwa na nikotini hasa au na nikotini pamoja na kemikali nyingine ndani ya moshi.
Hasara zilizotazamwa ni kama vile:
- hamu ya kula inapungua
- asidi inaongezeka tumboni
- maumivu ya kichwa
- mishipa ya damu hujikaza; inaonekana kuna uhusiano na mishipa myembamba kati ya wavutaji wa miaka mingi
Picha
hariri-
Muundo wa kikemia wa nikotini
-
Molekuli ya nikotini
Viungo vya nje
hariri- Description of nicotine mechanisms
- Erowid Nicotine Vault : Nicotine Material Safety Data Sheet
- CDC – NIOSH Pocket Guide to Chemical Hazards
Makala hii kuhusu mambo ya kemia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Nikotini kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |