Salah ad-Din
Salah ad-Din al-Ayubi (pia: Saladin: 1138 – 4 Machi 1193) alikuwa mtawala wa Misri na Syria wakati wa karne ya 12. Anakumbukwa hasa kwa ushindi wake juu ya Wamisalaba na ufalme wao wa Yerusalemu.
Aliunda nasaba ya Waayubi walioendelea kutawala Misri pamoja na Yemeni, Shamu, Iraq na Hijaz.
Kupanda ngazi kama mwanajeshi
Alizaliwa katika familia ya Wakurdi; babake alikuwa mwanajeshi katika utumishi wa Sultani wa Dameski. Alipokuwa na umri wa miaka 25 alitumwa Misri kwa vita dhidi ya Khalifa wa Wafatima. Huko Misri alipanda ngazi akawa waziri au mkuu wa serikali ya Misri.
Sultani wa Misri
Baada ya kifo cha khalifa wa mwisho, Salah ad-Din alitwaa mamlaka akajipa cheo cha Sultani na kutawala Misri.
Kutwaa Shamu na Yerusalemu
Mwaka 1174 alivamia Shamu na kuunganisha Syria na milki yake akaipanua hadi Aleppo (1183) na Mosul (1186) akaendelea kushambulia ufalme wa Yerusalemu wa Wamisalaba.
Tarehe 4 Julai 1187 alishinda jeshi lao na kutwaa mji wa Yerusalemu akimaliza utawala wa Wakristo uliowahi kudumu miaka 88.
Vita ya tatu ya Wamisalaba
Mataifa ya Ulaya yalikusanya jeshi jipya dhidi yake na kwenda kwa vita ya tatu ya misalaba. Mwaka 1191 Mfalme Richard I wa Uingereza alimshinda Salah ad-Din na pande zote mbili walipatana kupumzisha silaha. Walipatana ya kwamba Yerusalemu itabaki mikononi mwa Waislamu lakini Wakristo watakuwa huru kuhiji huko na kutembelea mji pamoja na mahali pa kumbukumbu ya Yesu. Ufalme wa Wamisalaba uliendelea kushika kanda la pwani la Palestina.
Kifo mjini Dameski
Tarehe 3 Machi 1193 Salah ad-Din aliaga Dunia mjini Dameski akiwa na umri wa miaka 55. Kaburi lake limetunzwa hadi leo: liko kando ya msikiti wa Umawiya.
Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Salah ad-Din kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |