Dar 2 Lagos
Dar 2 Lagos | |
---|---|
Posta ya Dar 2 Lagos | |
Imeongozwa na | Femi Ogedegbe |
Imetayarishwa na | Mtitu Game |
Imetungwa na | Steven Kanumba |
Nyota | Steven Kanumba Emmanuel Myamba Mercy Johnson Nancy Okeke Abdul Ahmed |
Imetolewa tar. | 30 Novemba, 2006 |
Ina muda wa dk. | 156 |
Nchi | Tanzania Nigeria |
Lugha | Kiswahili Kiingereza |
'Dar 2 Lagos ni jina la filamu iliyotoka mwaka 2006 kutoka nchini Tanzania. Ndani yake anakuja Mercy Johnson, Steven Kanumba, Bimbo Akintola, David Manento, Nancy Okeke, Blandina Changula,Abdul Ahmed na Emmanuel Myamba. Hii ni filamu ya kwanza kutoka Tanzania yenye kushirikisha wasanii kutoka Nigeria. Tangu hapa, ikawa kawaida sana kwa Kanumba kushirikiana na wasanii wa Nigeria. Filamu imeongozwa na Femi Ogedegbe kutoka Nigeria na kutayarishwa na Mtitu Game. Muswaada andishi ni kazi ya Kanumba ambaye ndiye aliyetunga hadithi ya filamu huu. Filamu inahusu ndugu wawili wa baba mmoja lakini mama tofauti wanajikuta wanaweka mahusiano ya kimapenzi, hatimaye wanajua kuwa wao ni ndugu na suala la ndoa linakufia hapo. [1] Filamu imetengenezwa na Game First Quality Production ya William Mtitu. Filamu ilizinduliwa katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam kwa burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii tofauti wa maigizo na muziki wa dansi walikuwepo Twanga Pepeta na Twanga Chipolopolo.[2]
Hadithi
[hariri | hariri chanzo]Filamu inaanza Kanumba anaingia duka la kuuza DVD tayari kwa kupata nakala kwa ajili ya kujitafutia riziki yake. Anachukua mzigo kisha anarudi kijiweni kwake na kugawiana na wenziwe ili kila mmoja akajifutie. Baadaye anaonekana Kelvin (Abdul Ahmed) akipigana na mmoja kati ya watu ambao Kanumba anawatumia kuuza CD. Anaamulia ugomvi ule na kuwafanya waondoe hasira zao na kuwa furaha. Jambo hili linamvutia Mzee Maganga (Manento) na kumsifu aendelee na moyo huo. Nyumbani kunaonekana malumbano ya kwenda kazini kati ya Kelvin na Kanumba, hatima Kelvin kagoma licha ya kusaidiwa. Kanumba aliyechangikiwa anaongea peke yake njiani akitafakari ya Kelvin, pembezoni mwa mtaa Mzee Maganga anamwona na kumsimamisha Kanumba.
Kama kawaida yake, alimpa usia na mwisho wa siku alimwalika nyumbani kwake. Huko nyumbani Kanumba anashangazwa na ukubwa wa nyumba na jinsi Mzee Maganga anavyojiweka mtaani. Maganga anamhadithia Kanumba kuwa yeye ni mwanajeshi mstaafu aliyetumikia sehemu mbalimbali. Maganga anaendelea kumhadithia Kaumba ya kwamba aliwahi kuoa mke wa Kinigeria na kuzaa watoto wawili wa kike, lakini hawajadumu sana katika ndoa akaondoa kwao Nigeria. Vilevile ana mtoto wa kiume ana Raymond ambaye mama yake ni Mtanzania. Yule wa Kinigeria aliondoka Nigeria na mabinti zake wote wawili.
Siku kadhaa mbele, Mzee Maganga anamwomba Kanumba aende Nigeria kuwatafuta watoto zake ili aweze kutambulishwa Kanumba katika familia. Anamwelezea Raymond nae yupo Nigeria kaenda kutafuta maisha. Kanumba anaenda kushauriana na nduguze juu ya safari, marafiki na mpenzi wake wanabariki safari. Lakini Kelvin bado anatia kinyongo kwa kumtia maneno ya hofu dhidi ya safari na na nia ya dhati ya Mzee Maganga. Hatimaye Kanumba anasafiri Nigeria na kufikia hoteli ambayo Mzee alimtaka afikie. Huko Nigeria, anaonekana Raymond na mpenzi wake ambaye anamdoea waoane, lakini binti anaona bado mapema na Raymond hakuwa mwazi katika maisha yake yeye na wazazi wake. Azimio linapita la kuchunguzana na hakuna kutenda lolote bila ndoa.
Kanumba anakuwa mwenyeji hotelini pale, anajenga urafiki wa karibu na Stella ambaye ni meneja wa hoteli ile. Stella anaomba kwenda matembezi na Kanumba, anakubali, lakini anakumbuka alitakiwa asafishe picha ambazo alipewa vivuli vyake na Mzee Maganga - picha ambazo zingemsaidia kuwatambua hao nduguze aliokuja kuwatafuta. Bahati mbaya zimefagiwa na msafishaji wa hotelini. Stella anamtuliza, na kumhisihi waende matembezi. Huko kwa Raymond na mpenziwe, kimenuka. Raymond anawaka, bado hataki kuwa mwazi ila anapayuka kwanini hakuna uroda mpaka kuoana. Msimamo wa Ester ni lazima Raymond amtambulishe kwa wazee wake. Raymond anaonekana kushikilia misimamo yake isiothabiti. Siku inayofuta Kanumba anaanza safari ya kutafuta anwani aliyopewa na Mzee Maganga ili ajue ni wapi walipo dada zake. Bila mafanikio, anaamua kurudi hoteli. Huko hotelini, anakuja yule binti aliyemsaidia siku za mwanzo katika kumpatia chakula ambacho hakina pilipili nyingi (Shola).
Shola, anaonesha mahaba ya waziwazi kwa Kanumba, lakini Kanumba haoneshi kukubaliana na hilo. Wanatoka ote nje kwa ajili ya chakula cha mchana. Nyumbani kwa kina Ester, Raymond asiyechoka, anaenda na gea ya kutaka kumvisha pete ya uchumba Ester, lakini inashindikana kwa vile Ester kabaki na misimamo yake thabiti ya bila wazee kutambulishwa hakuna ndoa. Punde, anaingia Stella na Kanumba, wanatambulishana. Ester anamlalamikia dada yake anachofanya Raymond, Stella anakomaa kama mdogo mtu anavyotaka au kama vipi ndoa isiwe. Chumbani, Stella anamsejuzi Kanumba ahamie kwake badala ya kukaa hotelini. Kanumba anamtosa, anaona ni udume suruali kwa Mtanzania kukaa kwa mwanamke. Hatimaye Kanumba kalegeza na kuamua kumsaliti mpenzi wake wa Tanzania kwa kwenda kuishi na Stella.
Jioni yake, wote wanne wanaaenda matembezi, huko Baa, mashauzi ya lugha za Kiswahili yanaanza, Stella, Ester na Kanumba wanatia maneno ya Kiswahili katikati ya maongezi. Mabinti wanaenda faragha, wanabaki wanaume, punde ukweli unakuwa uchi kwa Raymond kujitambulisha kama yeye ni Mtanzania kabisa huku akimtaka Kanumba afanye siri maongezi yao. Kanumba anaendelea na kuwatafuta nduguze bila mafanikio. Anampigia simu mzee na kumfahamisha anataka kurudi, katika maongezi anataja majina ya Kitanzania ya Misoji na Mihayo Maganga, Stella anastuka na kumwuliza unawajua hao unaosema ni marafiki kwa macho? Kanumba anajibalaguza, bila majibu yaliyonyooka anaamua kwenda kupumzika. Mazungumzo baina ya Kanumba na Raymond yanaendelea vizuri kwa kufunguka kupita maelezo. Mahusiano ya Kanumba na Stella yanaingia doa baada ya Kanumba kuwa anapiga simu zenye kutia mashaka kwa Stella. Simu zimegubikwa na usiri mzito kiasi kumvuruga Stella na kupitisha azimio la kutaka kila mtu aende na zake lakini Stella anaamua kuwa mpole ili kulinda pendo.
Kanumba kaendelea na usiri wake hadi kufikia hatua ya kupekua vitu vya chumbani kwa Stella, hilo limemuuma Stella. Kanumba katimuliwa nyumbani kwa Stella nakuamua kurudi hotelini. Siku ya pili Kanumba kaatisha kikao kwa wanne wale, Raymond, Stella na Ester na kuelezea kila kitu na kipi kilichomleta. Hatimaye ukweli unakuwa wazi na Ester anajua kama Raymond ni kaka yake. Vilio vinaanza na majonzi mazito miongoni mwao. Kanumba anaomba msamaha kwa wenzie, anawaelezea aliagizwa awe msiri katika safari hii. Isingekuwa rahisi kutoa au kulezea kila aliloazimia na mzee. Pia mzee anawataka warudi. Raymond anaambiwa mzee amekusamehe siku nyingi. Anatakiwa arudi nyumbani. Stella anaazimia kuvunja uchumba wa Raymond na Ester. Anawaambia ni mwiko kuoana kwa kaka na dada. Kanumba anamwomba msamaha Stella kwa yote aliyoyafanya na bado anampenda kwa dhati kutoka moyoni. Picha inaishia Kanumba na Raymond wanarudi Tanzania, Ester na ahadi za kurudi Tanzania ili kumuona baba yake na ujumbe wa kuwa bado anampenda baba yake. Shola kaachwa kwenye mataa baada ya kwenda hoteli na kukutana na barua ya Kanumba inayomwomba msamaha wa kuondoka bila kumuaga.
Washiriki
[hariri | hariri chanzo]- Mercy Johnson
- Steven Kanumba
- Bimbo Akintola
- David Manento
- Abdul Ahmed
- Nancy Okeke
- Blandina Changula
- Emmanuel Myamba
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Dar 2 Lagos Archived 7 Juni 2017 at the Wayback Machine. katika Bongo Cinema.com
- ↑ uzinduzi wa Dar 2 Lagos Dar es Salaam mnamo 30 Novemba, Diamond Jubilee.