Location via proxy:   [ UP ]  
[Report a bug]   [Manage cookies]                
Nenda kwa yaliyomo

Mkoa wa Mara

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mkoa wa Mara
Mahali paMkoa wa Mara
Mahali paMkoa wa Mara
Mahali pa Mkoa wa Mara katika Tanzania
Majiranukta: 1°33′S 34°1′E / 1.550°S 34.017°E / -1.550; 34.017
Nchi Tanzania
Wilaya 7
Mji mkuu Musoma
Serikali
 - Mkuu wa Mkoa Mh. Kanali Enos Mfuru
Eneo
 - Jumla 30,150 km²
 - Maji 7,500 km² 
Idadi ya wakazi (2022)
 - Wakazi kwa ujumla 2,372,015
Tovuti:  http://www.mara.go.tz/

Mkoa wa Mara ni kati ya mikoa 31 ya Tanzania wenye postikodi namba 31000.[1].

Umepakana na mikoa jirani ya Mwanza na Shinyanga upande wa kusini, Arusha upande wa kusini-mashariki, Kagera kwa njia ya Ziwa Nyanza (au Viktoria) na Kenya upande wa mashariki.

Jina linatokana na lile la mto Mara.

Musoma ndio makao makuu ya mkoa.

Idadi ya wakazi ilikuwa 2,372,015 wakati wa sensa ya mwaka 2022[2], kutoka 1,743,830 wa sensa ya mwaka 2012 [3], na 1,368,602 wa sensa ya 2002[4].

Kuna wilaya 9 zifuatazo katika mkoa wa Mara: Bunda Mjini, Bunda Vijijini, Serengeti, Tarime Vijijini, Tarime Mjini, Rorya, Butiama, Musoma mjini na Musoma vijijini.

Sehemu kubwa ya Hifadhi ya Wanyama ya Serengeti iko ndani ya Mkoa wa Mara.

Makabila

Kaburi la baba wa taifa Julius Kambarage Nyerere mjini Butiama.

Makabila ya Mara ni mengi kuliko mikoa yote ya Tanzania, kama vile Waluo, Wajita, Waruri, Wazanaki, Wakuria, Wakabwa, Wakiroba, Wasimbiti, Wangoreme, Wakwaya, Waikoma, Wanata, Waisenye, Waikizu, Wasizaki, Wasukuma, Wataturu na makabila madogo kama Wanandi, Wakisii au Wamaragori.

Kuna jumla ya makabila 30 yanayodai kujitegemea. Jamii zinazosahaulika huunganishwa katika kundi la Suba (Wategi, ambao pia huitwa Abhathegi maarufu kama Abhagirango, Waugu (Ugu), Warieri, Wakine, Wasweta na Waganjo, Wagire, Wakiseru, Wakamageta na Waturi). Baadhi ya jamii hizi zilimezwa na mila, lugha na desturi za Waluo zikaitwa Suba-Luo katika kipindi cha utawala wa DC Engram aliyekuwa wilaya ya Mara Kaskazini (North Mara).

Baadhi ya jamii kwa upande wa Kenya iliyotawaliwa na Waingereza katika Wilaya za Kuria na South Nyanza huitwa Suna, Wagwasi, Ungoe, Kajulu na Kadem.

Hata hivyo habari hizi bado zinafanyiwa utafiti kuangalia muingiliano wa lugha na tofauti za kilahaja kati ya jamii moja na nyingine hasa zilizopo Tanzania. Itakumbukwa jamii nyingi ziliingia upande ulioitwa South Nyanza kabla ya nchi za Afrika Mashariki kupata uhuru. Zipo tafiti nyingi siku hizi ambazo zinajaribu kubainisha makundi ya jamii hizo lakini muingiliano bado haujapata ufafanuzi makini.

Kimsingi Mkoa wa Mara una jamii hizo zipatazo 30 lakini lugha kuu ni saba tu na nyingine ni lahaja kutokana na makundi ya lugha hizi: Luo, Kuria, Sukuma, Suba, Shashi, Zanaki na Taturu. Yapo makundi ya Wanata, Waisenye na Wataturu, Wazanaki (kundi lake: Kabwa, Kirobha, Wasimbiti, Wairienyi, Waikizu, Wangoreme), Luo (Wakowak, Wakamoti), Wakuria (Nyebhasi, Nyamongo, Wanchari, Wasweta, Wakenye, Warenchoka, Watimbaru, Waregi, hadi 14/15), Sukuma, Nyantuzu na Shashi (Wajita, Wakwaya, Waruri, Wakerewe, Wakara). Jamii zote humezwa katika makundi saba ya lugha kuu lakini kila jamii inajitofautisha kwa lahaja yake.

Ni jamii za Kibantu peke yake zinazoweza kuwasiliana na kuelewana kukiwa na tofauti kidogo katika matamshi ya maneno.

Ukichunguza zaidi, wakazi wa asili wa Mkoa wa Mara ni makabila makuu mawili yenye uhusiano wa karibu sana, yaani Wakurya (na vikabila kadhaa: Wakurya ni jina ‘linalobeba’ mengi ya yale yanaoyoitwa 'makabila' mkoani Mara, ambayo tafsiri yake halisi ni 'vikabila'[5]) na Wajita (hawa nao wana vikabila kadhaa).

Pia, Wakurya-Waghusii si 'Bantu halisi' bali ni mchanganyiko kati ya Wabantu na Waniloti. Katika makabila ya Kibantu, yaliyoathiri damu ya Wakurya ni pamoja na:

  • Wasukuma (kwa mfano, baadhi ya koo za Kizanaki, zilichanganya damu sana na Wasukuma)
  • Wachaga (kwa mfano, Wakerobha au Wakiroba, walichanganya damu sana na wahamiaji toka Machame na Marangu kwa Wachaga - na hadi leo Machame na Marangu ni majina ya vitongoji huko kwa Wakiroba Mkoa wa Mara!)
  • Wakikuyu (kwa mfano, baadhi ya Wakurya wa North Mara wana asili ya Wakikuyu au 'Abhaghekoyo'). Pia Wakikuyu wanachanga majina mengi na Wakurya - kama Nyambura, Murughi, Mwita, n.k. na hata lugha zinafanana kwa kiasi kikubwa).

Pia, kama makabila, Wakurya-Waghusii, Wakikuyu, na Wameru wa Kenya wana uhusiano wa karibu na asili moja. Makabila mengine yanayohusiana nao ni Wagisu (Uganda) na Waluya (Kenya). Kuna wakati ambapo makundi hayo yote yalikuwa kabila moja, lakini wakatengana kwa kuhamia sehemu za mbali, wakawa makabila tofauti tunayoyajua leo.

Waniloti waliochanganya damu na Wakurya ni pamoja na:

  • Wamasai (baadhi ya koo za Wakurya wa leo zilitoka Umasai).
  • Wajaluo (hasa kutokana na kuona kwani, tokea ujio wa Waniloti Mkoani Mara, watu hawa ni majirani),
  • Wakalenjin (hasa kutokana na uhamiaji na wote kuwa na mila za wafugaji).

Kwa hiyo, dhana ambayo imejengeka sana vichwani mwa watu kwamba Mara kuna makabila mengi, kwa kiasi kikubwa ni potofu. Ukiangalia kwa undani hata lugha na mila zilizopo, utaona kwamba hata hao kina yego/mbani (Wajita, Wakwaya, Wakara, Waruri, Wakerewe, n.k.) ni 'vikabila' tu vya kabila kubwa la Wajita.

Ukiachia Wajaluo (au 'Jakowiny Luo'), mkoani Mara pia kuna Wataturu na Wanandi. Wanandi ni moja kati ya 'vikibila' vya Wakalenjin. Hata hivyo, idadi ya watu wa makabila haya ni ndogo ukilinganisha na ile ya 'Wakurya-Waghusii' na Wajita (ikiwa na maana ya kabila kubwa linalojumuisha pia Wajita, Wakwaya, na Waruri).

Pia Mara, Wakurya hawaishi tu Tarime, bali huishi wilaya zote 6 za Mkoa wa Mara: Tarime, Rorya (hao ni Wakurya wa North Mara), Musoma Vijjini, Musoma Mjini, Bunda, na Serengati (hao ndio Wakurya wa South Mara). Abhaghusii (wanaoishi jimbo la Nyanza, Kenya) ni sehemu ya Wakurya wa 'North Mara'.

Kwa hiyo, wanahistoria wanatakiwa kuliweka hili sawa. Wazungu walichorekodi ni majina ya vikabila (au koo kubwa), kwani hata leo ukienda Mara, ukauliza swali lako kizembe, si ajabu usikute mtu atayekujibu kwamba anaitwa Mkurya: wote watakuambia, mimi Mzanaki, Mkiroba, Mtimbaru, n.k. Wengine watasema, mimi Mmjita, Mkwaya, Mruri, nk.

Kwa wakereketwa wa historia, Wakiroba (kikabila cha Wakurya-Wakisii) na Wakwaya (kikabila cha Wajita) ndiyo makabila ya asili ya inayoitwa leo hii Musoma mjini. Makundi haya mawili, pamoja na kuwa makibali tofauti, yana uhusiano wa muda mrefu wa karibu sana. Hupendana sana, na hata vita walipigana kwa kushirikiana!

Pia Wakurya na Wajita, uhusiano wao wa karibu, na hata kushabihiana kwa lugha zao (kwa makabila haya makubwa mawili ya Mkoa wa Mara, hakuna anayeweza akamsengenya mwenzie, na asijue anasema nini), si jambo lililoanza juzi. Mababu wanatuambia hawa watu wote wamehamia Mara, wakitokea maeneo ambayo kwa sasa yako katika nchi zinazojulikana kama Misri na Libya (hata Wajaluo nao, walikujua toka huko). Wakati wa msafara, waligawanyika makundi matatu:

• Moja likapita mashariki mwa Ziwa Victoria. Hili lilikuwa ndilo kundi kuu. Koo nyingi za Kikurya zilipita huko. Katika nyakati tofauti, zilitengana na Wagisu (Uganda), Waluya, Wameru, Wakikuyu (Kenya).

• Moja likapita magharibi mwa Ziwa Victoria. Koo nyingi za Wajita, pamoja na baadhi ya koo za Wakurya (kama Abhashanake) walipita huko.

• Moja likapita katikati ya Ziwa Victoria. Hili kundi lilikuwa dogo zaidi. Lilijumuisha zaidi koo chache za Kijita, kama vile Wakerewe.

Hakuna historia ya vita kati ya Wakurya na Wajita, bali wameishi kwa kuelewana na kusaidiana. Hata hivyo, koo za Kikurya hupenda sana kupigana – na haya tunayaona hadi leo hii.

Pia tukumbuke: Wabantu ni familia moja, na Waafrika ni ’kabila’ moja kubwa, na binadamu wote, bila kujali rangi zetu, tumetoka kwa Muumba mmoja na tuna asili moja – ni watoto wa Adamu na Eva (Waarabu humwita Hawa), kwa wale wanaoamini dini; au ni watoto wa Mwafrika kwa wale wanaoamini sayansi.

Majimbo ya bunge

Wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2015 mkoa huu ulikuwa na majimbo ya uchaguzi yafuatayo:

Tazama pia

Marejeo

  1. https://sw.wikipedia.org/wiki/Mfumo_wa_Msimbo_wa_Posta_Tanzania
  2. https://www.nbs.go.tz
  3. Sensa ya 2012, Mara Region
  4. "Mara Region Homepage for the 2002 Tanzania National Census". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2003-12-15. Iliwekwa mnamo 2003-12-15.
  5. Kwa hiyo unapotaja 'vikabila' vya Wakurya, kwa usahihi, utataja, pamoja na vinginevyo: Abhatimbaru (Watimbaru), Abhakira (Wakira), Abhanyamongo (Wanyamongo), Abhasubha (Wasuba), Abhakerobha (Wakiroba), Abhakabhwa (Wakabwa), Abhasimbete (Wasimbiti), Abhaikoma (Waikoma), Abhangoreme (Wangoreme), Abhaisenye (Waisenye), Abhanyabhasi (Wanyabasi), Abhaireghe (Wairege) n.k. bila kuwasahau Abhaghusii (Wakisii). Kihistoria, Wakurya (Abhakurya, Abhakorya) na Wakisii ('Waghusii' au 'Abhaghusii' tukitumia maneno sanifu katika lugha husika) ni kabila moja. Tofauti ndogo zilizopo katika lugha ni za kijiografia tu. Hata Abhashanake (Wazanaki), Abhaighisho (Waikizu), Abhanatta (Wanata), n.k. ni 'vikabila' tu vya Wakurya. Makundi yote hayo ni makundi ya 'Mura' (sawa na Morani kwa Wamasai) na 'Bhei' (kwa jinsia ya kike). Tamaduni zao ni zilezile - kutahiri wanawake kwa wanaume, kuchonga meno (hata Mwalimu jina lake la utani ni 'Mchonga'), kuwa na sera ya Marika (kama Abhaghini, Abhanyambureti, etc.) yanayozunguka vizazi hata vizazi na kujirudia, kuwa na 'Ekesero' kama kundi la watu waliotahiriwa wakati mmoja, ambao hlikuja kuwa msingi wa majina ya 'intakes' za JKT), n.k.

Viungo vya nje


Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Mara bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Mkoa wa Mara kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.

Usiingize majina ya viongozi au maafisa wa sasa maana wanabadilika haraka mno.