Location via proxy:   [ UP ]  
[Report a bug]   [Manage cookies]                

Mfereji wa Suez (kwa Kiarabu: قناة السويس, qanā as-suways) ni mfereji mkubwa nchini Misri.

Manowari ikipita katika Mfereji wa Taabah Rafah Straights.
Mfereji wa Suez kutoka angani kati ya Mediteranea (juu) na Bahari ya Shamu (chini).

Mahali pake

hariri

Unaunganisha Bahari ya Mediteranea na Bahari ya Shamu, hivyo na Bahari Hindi pia.

Mfereji uko upande wa magharibi wa rasi ya Sinai. Urefu wake ni km 163 na upana ni kuanzia mita 300.

Unaanza mjini Port Said (Būr Sa'īd) upande wa Mediteranea na kuishia mjini Suez (al-Suways) upande wa Bahari ya Shamu.

Historia

hariri

Ulijengwa na kampuni ya Kifaransa kati ya miaka 1859 na 1869.

Kuna mifereji mbalimbali iliyotangulia huko kuanzia karne ya 14 KK hadi wakati wa Waarabu katika karne ya 8 BK. Lakini yote haikudumu kwa sababu ya matatizo ya kuondoa mchanga mara kwa mara kwa mitambo iliyopatikana zamani. Tena katika mifereji ya zamani ilikuwa serikali ya Misri tu iliyotaka kurahisisha usafiri na ubebaji wa mizigo.

Tangu kupatikana kwa meli za kisasa idadi ya meli kati ya Ulaya na Asia iliongezeka sana katika karne ya 19. Zote zilipaswa kuzunguka Afrika yote au kuondoa mizigo na abiria upande wa Mediteranea na kuwasafirisha hadi Suez. Hivyo ilikuwa jitihada ya kimataifa yaliyoleta mfereji wa kisasa.

Meli ya kwanza ilipitia mfereji mpya tarehe 17 Februari 1867. Mtunzi wa muziki Giuseppe Verdi aliandika opera yake Aida hasa kwa nafasi hiyo.

Umuhimu wa mfereji wa Suez

hariri
 
Njia za usafiri baharini kabla na baada ya kupatikana kwa Mfereji wa Suez

Mfereji wa Suez unafupisha umbali wa safari ya meli kati ya Ulaya na Asia kwa kilomita 8,000 hivi; kwa mfano safari baina ya Rotterdam (bandari kubwa ya Ulaya) na Dubai ni takriban kilomita 20,900 na siku 24 kwa njia ya kuzunguka Afrika; kupitia Mfereji wa Suez ni kilomita 12,000 na siku 12 pekee.[1] Mfereji umeharakisha na kurahisisha usafiri kati ya Ulaya, Asia na Afrika ya Mashariki. Zipatao meli 15,000 zinapita kwenye mfereji kila mwaka.

Mafanikio ya mfereji wa Suez yalihamasisha mianzo ya Mfereji wa Panama.

Kutaifishwa kwa mfereji 1956

hariri

Mfereji ulikuwa mali ya Compagnie universelle du canal maritime de Suez au kampuni ya mfereji wa Suez na hisa zake zilikuwa mikononi mwa serikali za Ufaransa na Uingereza.

Mwaka 1956 serikali ya Misri chini ya rais Gamal Abdel Nasser ilitaifisha mfereji na tendo hilo likasababisha vita ya Suez ya 1956 ambako Uingereza, Ufaransa na Israel zililazimishwa na mataifa makubwa kujiondoa katika Misri baada ya uvamizi wao.

  1. "The Suez Canal - A vital shortcut for global commerce" (PDF). World Shipping Council. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2018-04-22. Iliwekwa mnamo 2020-09-11.