Mara (kundinyota)
Kwa matumizi tofauti ya jina Mara angalia hapa Mara (maana)
Mara ni kundinyota linalojulikana pia kwa jina lake la kimagharibi la Andromeda[1]. Ni moja ya makundinyota yanayotambuliwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [2] Jinsi ilivyo kwenye makundinyota yote, nyota za Mara hazikai pamoja hali halisi lakini zinaonekana vile tu kutoka duniani. Hali halisi kuna umbali mkubwa kati yao. Kwa hiyo "Mara" inataja eneo la angani jinsi linavyoonekana kutoka Dunia.
Jina
Mara lilijulikana kwa jina hili kwa miaka mingi kati ya mabaharia Waswahili walioitumia kutafuta njia baharini wakati wa usiku.[3]
Jina la Mara linatokana na kifupi cha Kiarabu المرأة المسلسلة al-marʾa(t) al-musalsala ambalo linamaanisha "mwanamke aliyefungwa kwa nyororo ". Jina hili lilipokelewa na Waarabu kutoka kwa mitholojia ya Wagiriki wa Kale walioziita nyota hizi Ανδρομέδα ("Andromeda") kufuatana na masimulizi ya binti wa mfalme aliyefungwa kwa nyororo kwenye ufuko wa bahari ili aliwe na dubwana wa baharini lakini aliokolewa na Farisi (Perseus). Hadithi hii ina mizizi katika mitholojia ya Babeli. [4].
Mahali pake
Mara linaonekana pande zote mbili za ikweta ya Dunia; katika Afrika ya Mashariki Mara linaonekana kuanzia Septemba hadi Februari. Inapatikana juu ya nyota zinazokaa kwa umbo la herufi "M“ ya kundinyota Mke wa Kurusi (Cassiopeia) na karibu na Farasi (Pegasus) kwa upande wa magharibi na Farisi (Perseus) upande wa mashariki.
Magimba ya angani
Sehemu ya Mara inayotambuliwa kirahisi ni safu ya nyota nne zinazotoka kwenye pembenne ya Farasi. Nyota tatu angavu zaidi zinaitwa γ Andromedae au Alamak, β Andromedae au Mirach na α Andromedae au Sirrah zikiwa kweye mstari usionyoka.
Upande wa kusini kati ya δ Andromedae na β Andromedae doa jeupe linaonekana ambalo ni galaksi M31 linalojulikana pia kama galaksi ya Andromeda. Hii ni galaksi ya karibu zaidi na Njia Nyeupe na Dunia.
Tanbihi
- ↑ Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Andromeda" katika lugha ya Kilatini ni "Andromedae" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Andromedae, nk.
- ↑ The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
- ↑ ling. Knappert 1993
- ↑ Allen, uk 31-32
Marejeo
- Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 252 (online kwenye archive.org)
- Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
- http://www.solarsystemquick.com/universe/andromeda-constellation.htm