Location via proxy:   [ UP ]  
[Report a bug]   [Manage cookies]                
Nenda kwa yaliyomo

Jiografia ya Urusi

Majiranukta: 60°N 100°E / 60°N 100°E / 60; 100
Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

60°N 100°E / 60°N 100°E / 60; 100

Map of Russia

Jiografia ya Urusi inaeleza tabia za nchi ya Urusi inayotanda juu ya maeneo mapana ya Eurasia ya kaskazini na ambayo ni nchi yenye eneo kubwa zaidi duniani, ikiwa na kilomita za mraba milioni 17.[1] Ina asilimia 11 za maeneo yote ya nchi kavu duniani ambayo ni sawa na jumla ya maeneo ya Ulaya na Australia.

Kutokana na ukubwa huo kuna tofauti sana ndani ya Urusi kuhusu tabianchi, uoto na aina za udongo.[2] Aina zote za tabianchi za dunia zinapatikana huko isipokuwa tabianchi za kitropiki.

Kutoka kaskazini kuelekea kusini kuna kanda zifuatazo zinazofuatana katika nchi kwa jumla:

Upande wa mashariki, yaani katika Siberia, kanda ya taiga (misitu) ni pana zaidi.

Urusi ina hifadhi ya biosferi 40 zilizokubaliwa na UNESCO.[3]

Mahali pa Urusi duniani na mipaka yake

[hariri | hariri chanzo]

Urusi yote iko kwenye nusutufe ya kaskazini ya dunia yetu na kwa jumla iko karibu zaidi na ncha ya kaskazini.

Kuanzia Kaliningrad upande wa magharibi hadi Kisiwa cha Ratmanov kwenye mlangobahari wa Bering upande wa mashariki kuna umbali wa kilomita 8,000.

Kutoka visiwa vya Aktiki vya Urusi kwenye kaskazini hadi Dagestan kwenye mwambao wa Bahari ya Kaspi upande wa kusini kuna umbali wa kilomiita 4500.

Mipaka ya Urusi huwa na urefu wa kilomita 57,792 na kilomita 20,139 ziko kwenye nchi kavu, nyingine ni mipaka ya baharini na pwani za nje. Kuna mipaka na nchi 14: Norwei, Ufini, Estonia, Latvia, Lithuania, Poland (mpaka na Kaliningrad Oblast), Belarus, Ukraina, Georgia, Azerbaijan, Kazakhstan, Mongolia, China na Korea Kaskazini.

Sehemu kubwa ya mipaka ya nje iko kwenye maji. Pwani ndefu zaidi ni ile ya kaskazini iliyopo ng'ambo ya Mzingo Aktiki; kwa hiyo pwani hiyo inafunikwa na barafu ya bahari kwa sehemu kubwa ya mwaka isipokuwa bandari ya Murmansk inayopokea maji fufutende kiasi kutoka mkondo wa ghuba. Bahari Aktiki, Atlantiki na Pasifiki zinagusana na pwani za Urusi.

Ina mipaka iliyopo baharini na Marekani, jimbo la Alaska na Japani, mkoa wa Hokkaido.

Bahari mpakani urusi - Bahari Nyeusi, Bahari ya Azov, Bahari Nyeupe, Bahari ya Barents, Bahari ya Kara, Bahari ya Laptev, Bahari ya Mashariki ya Siberia, Bahari ya Chukchi, Bahari ya Bering, Bahari ya Ohotsk na Bahari ya Japani.

Topografia

[hariri | hariri chanzo]

Eneo kubwa la Urusi hugawiwa kwa macho ya ekolojia kwa kanda asilia tano:

Maeneo makubwa ni uwanda, hasa uwanda wa Ulaya ya Mashariki na uwanda wa Siberia ya Magharibi, halafu nyanda za chini za Siberia Kaskazini na Kolyma. Nyanda za juu za Siberia ya Kati na Lena halafu safu za milima kwenye kaskazini-mashariki na kwenye mpaka wa kusini.

Kanda za uoto

[hariri | hariri chanzo]
Ramani ya tundra aktiki
Ramani ya Aktiki ya Kirusi

Sehemu ya Aktiki ya Urusi zinaenea karibu kilomita 7000 kuanzia Karelia na Rasi ya Kola upande wa magharibi hadi Nenetsia, Ghuba ya Ob, Rasi ya Taymyr na Rasi ya Chukchi (Kolyma upande wa mashariki.

Visiwa muhimu katika Aktiki ya Urusi ni pamoja na Novaya Zemlya, Severnaya Zemlya na funguvisiwa la Siberia Mpya.

Takriban asilimia 11 za maeneo za Urusi ni tundra, yaani uwanda bila miti, kutokana na udongo jalidi wa kudumu, inayojaa matope kipindi cha majirajoto. Hii ni kanda ya kaskazini ya Urusi kutoka mpaka na Ufini hadi mlangobahari wa Bering. Jua halionekani kwa wiki kadhaa mfululizo wakati wa majirabaridi lakini katika wiki za mwezi wa Juni hakuna usiku kamili.

Miti haiwezi kustawi kwa sababu udongo umeganda na jalidi ya kudumu haitoki ardhini. Kama miti iko inatokea kwa umbo la vichaka vidogo tu. Ni ganda la juu pekee linalopoa wakati wa joto na kuruhusu uoto wa manyasi, kuvumwani, kuvu na vichaka vichache vidogo. Wakati joto linapanda barafu ya juu inayeyuka lakini maji haiwezi kutiririka chini katika ardhi kwa hiyo nchi inajaa matope na mabwawa madogo.

Kilimo hakiwezekani na hivyo wakazi ni wachache, junma ni asilimia moja ya wananahi wa Urusi pekee. Tasnia ya uvuvi na bandari kwenye rasi ya Kola na uzalishaji wa gesi asilia na mafuta ya petrol katika Siberia ya Kaskazini Magharibi ni ajira ya wengi wao. Bandari ya Murmansk na mji wa viwanda Norilsk (wakazi 180,000) ni miji miklubwa kiasi ya pekee hapo katika tundra.

Taiga ni kanda inayoenea kutoka mipaka ya magharibi hadi Pasifiki upande wa mashariki na kuwa 60% za eneo la Urusi kwa jumla. Inafunikwa kwa theluji kwa miezi mingi ya mwaka. Miti yake ni hasa aina mbalimbali za misonobari. Kutokana na baridi kuna wanyama wengi wenye manyoya mazito kama vile dubu, fisi-maji, melesi, elki, vicheche, wolverini na wengine waliovindwa kwa sababu ngozi zao zilitafutwa sana kwa matumizi ya koti katika nchi zote zenye majirabaridi kali. Uwindaji huu ulikuwa muhimu kiuchumi na sababu muhimu kwa uenezaji wa Urusi katika Siberia.

Elki

Misitu mingine

[hariri | hariri chanzo]
Msitu wa mibetula karibu na Novosibirsk

Mbuga baridi

[hariri | hariri chanzo]

Mbuga baridi (kwa Kiingereza steppe) ni kanda ya nchi inayoenea kuanzia Ukraina kupitia Urusi ya kusini hadi Kazakhstan na Manchuria. Uoto wake ni manyasi bila miti; miti inaweza kutokea penye maji karibu na mito au maziwa. Lakini kwa jumla tabianchi ya kanda hii ni yabisi au nusuyabisi ni hasa ukame unaozuia uoto wa miti.

Ni eneo linalofaa kwa kilimo kutokana na rutba ya ardhi lakini maji ni tatizo.

Mbuga wa Urusi na Asia ya Kati ulikaliwa tangu miaka mielfu na wafugaji wahamiaji waliotembea hapa na makundi yao ya kondoo, mbuzi na farasi. Farasi walianza kufugwa hapo na kutumiwa kwa usafiri na vita. Mawimbi ya wahamiaji na wavamizi yalipita hapa katika historia na kuvamia nchi jirani, mashuhuri ni uenezaji wa milki ya Wamongolia na Waturuki.

Mito, maziwa, utiririshaji

[hariri | hariri chanzo]
Picha ya Ziwa Baikal kutoka angani
Mto Chusovaya ukujiunga na mto Kama karibu na mji wa Perm

Urusi ni nchi yenye maji mengi. Kuna mabeseni ya utiririshaji 20.

Mito mikubwa ilikuwa njia za kwanza za usafiri na mawasiliano. Mto Volga ni mto mrefu wa Ulaya na njia muhimu ya usafiri. Miji minne mikubwa (kati ya miji 13 mikubwa zaidi nchini) iko kando ya Volga: Nizhny Novgorod, Samara, Kazan na Volgograd. Mto Kama unaotoka milima ya Ural na kuelekea magharibi unapojiunga na Volga katika Jmahuri ya Tatarstan ni muhimu pia.

Kwa jumla kuna mito elfu kadhaa. Mingi iko sehemu ya beseni la utiririshaji la Aktiki ambako kuna watu wachache. Kwa hiyo sehemu kubwa ya maji haina matumizi kwa manufaa ya binadamu. Kinyume chake maeneo ya Urusi ya kusini penye vipindi vya joto na wakazi wengi yanaona vipindi vya uhaba wa maji kama vile mabeseni ya mto Don na mto Kuban.

Upande wa mashariki ya Ural kuna mito 40 yenye urefu unaozidi kilomita 1,000. Ni hasa mito 3 inayobeba maji ya Siberia kwenda Bahari Aktiki:

Mito hii mitatu humwaga kila sekunde m³ 50,000 kwenye Bahari Aktiki. Vyanzo vya maji viko kusini vikielekea kaskazini. Hii inasababisha kutokea kwa maeneo makubwa mno ya kinamasi kwa sababu theluji ya kusini inaanza kuyeyuka mapema na maji yanaongezeka kaskazini wakati huko ardhi bado imegandishwa kwa hiyo maji hayawezi kuingia ardhini na kufanya vianmasi vikubwa. Takriban asilimia 10 za uso wa ardhi ya Urusi ni kinamasi.

Kati ya maziwa makubwa kuna Ladoga, Onega karibu na Saint Petersburg, Ziwa Peipus kwenye mpaka wa Estonia na lambo la Rybinsk kaskazini ya Moscow. Ziwa la lambo la Bratsk ni kati ya malambo makubwa duniani.

Ziwa lenye kina kubwa duniani ni Ziwa Baikal inayoshika asilimia 85 ya maji matamu ya Urusi na asilimia 20 ya maji matamu duniani.

Tabianchi

[hariri | hariri chanzo]
Ziwa Baikal. Maji yananza kuganda upande wa kaskazini ya ziwa na kwenye hori ya katikati

Tabianchi ya Urusi ni hasa ya kibara kutokana na umbo la nchi na umbali wa sehemu nyingi na bahari. Maeneo mengi yana umbalio wa kilomita 400 na zaidi kutoka ufukoni, na kitovu cha nchi kipo kwa umbali wa 3840 na bahari.

Zaidi ya hayo Urusi ina safu za milima mirefu hasa upande wa kusini na upande mashariki inayozuia kufika rahisi upepo kutoka Bahari Hindi na Pasifiki mwenye uweyo wa kupoza halijoto. Kinyume chake upepo kutoka Bahari aktiki unaweza kuingia bila vizuizi vya aina hii.

Ilhali zaidi ya nusu ya nchi iko kaskazini ya latitudo ya 60° sehemu kubwa hufunikwa kwa theluji kwa muda miezi sita. Chini yake iko ardhi kwenye hali ya jalidi ya kudumu kwa kina cha mita mamia. Halijoto ya wastani ya sehemu kubwa ya Siberia iko chini ya 0°.

Sehemu kubwa za Urusi zinaona majira mawili tu ambayo ni majirajoto na majirabaridi yenye jeledi. Vipindi vya kati ni vifupi sana. Hii inaathiri pia njia za usafiri. Wakati wa majirabaridi ambako maji yote kwenye mito na maziwa yanaganda barabara zinafunguliwa juu ya barafu ya mito mikubwa au kupitia maziwa makubwa.

Kuna maeneo machache ambayo hayafuati maelezo haya, ni eneo la Kaliningrad Oblast kwenye pwani la Bahari Baltiki pamoja na sehemu zilizo karibu na Pasifiki katika Mashariki ya Mbali. Kanda nyembamba la pwani kwenye Bahari Nyeusi huwa na tabianchi nusutropiki.

Wakati wa Januari halijoto ni −6°C huko Saint Petersburg, −27 °C katika Siberia ya magharibi na −43 °C huko Yakutsk katika Siberia ya Kati. Wakati wa majirajoto halijota inapatikana kati ya wastani ya 4 °C kwenye visiwa vya aktiki na wastani ya 20 °C katika kusini.

Halijoto ya chini iliyopimwa ilikuwa −68 °C huko Siberia ya kaskazini na +45 °C katika kusdini ya nchi.

Ukali wa baridi ina athari kubwa juu ya maisha yote, jinsi gani watu wanaweza kufanya kazi na kama kilimo kinawezekana au la. Majengo yanapaswa kuwa na tabia za pekee hasa katika maeneo ya jalidi ya kudumu ambako ni lazima kuweka kila jengo juu ya nguzo zinazofikia kina cha jalidi kwa sababu uso wa ardhi inakuwa laini na matope wakati wa joto; mashine zinapaswa kutengenezwa kwa kutumia feleji inayovumilia tofauti kubwa za jalidi na joto.

Miezi ya jalidi ni pia kipindi cha giza kwa hiyo kuna mahitaji ya pekee ya nishati na nguo.

Usimbishaji katika sehemu nyingi za Urusi si mkubwa kwa sababu maeneo mengi yako mbali na pwani na hivyo hayapokei hewa yenye unyevunyevu kutoka bahari.

Sehemu zinazopokea mvua nyingi ziko karibu na pwani kama Sochi kwenye Bahari Nyeusi (1500 mm kwa mwaka) na visiwa vya Kurili (1000 - 1500 mm, hasa theluji). Pwani la Baltiki lapokea 600 mm, Moscow 525 mm kwa mwaka. Maeneo yaliyo karibu na Kazakhstan hupokea 20 mm kwa mwaka pekee, na kwenye sehemu za pwani za Aktiki ni 15 mm pekee.

Theluji hufunika uso wa ardhi kati ya siku 40 hadi 200 kwa mwaka katika Urusi ya magharibi, na siku 120 - 200 kila mwaka katika Siberia.

Eneo na mipaka

[hariri | hariri chanzo]

Eneo (bila Krim):

  • Jumla: 17,098,242 km²
  • Nchi kavu: 17,021,900 km²
  • Maeneo ya maji: 79,400 km²

Urefu wa mipaka yote

  • Jumla (bila Krim): 19,917 km

Kaliningrad ni sehemu ya magharibi kabisa tangu 1945; ni eneo la pekee iliyotengwa kijiografia na sehemu nyingine za Urusi, iko ng'ambo ya Lithuania.

Krim ni rasi kwenye Bahari Nyeusi inayotazamiwa kuwa sehemu ya Ukraina na jumuiya ya kimataifa lakini ilijitega katika uasi wa 2014 na kutekjwa na Urusi kwenye Machi 2014.

Nchi zinazopakana:

Jumla ya pwani zote (bila Krim): 37,653 km

Malighafi na matumizi ya ardhi

[hariri | hariri chanzo]

Urusi ina akiba kubwa za malighafi duniani katika ardhi yake kushinda nchi zote nyingine. Tatizo ni ziko mara nyingi katika maeneo penye tabianchi ngumu hasa baridi kali na tofauti kali za joto na baridi kwa hiyo ni vigumu kuzilima.

Urusi ina fueli za kisukuu tele, labda nusu ya makaa mawe yote duniani na pia mafuta ya petroli mengi. Akiba za gesi asilia ni asimila 40 za jumla ya duniani.

Matapo ya metali nyingi hupatikana:

Takriban asilimia 8 za ardhi hulimwa, asilimia 4 ina matumizi kama lishe ya ufugaji, asilimia 64 ni misitu.

  1. "Russia". Encyclopædia Britannica. Iliwekwa mnamo 2008-01-31.
  2. "Russia::Climate and vegetation". Encyclopædia Britannica. Iliwekwa mnamo 2007-07-03.
  3. The World Network of Biosphere Reserves — UNESCO. "Russian Federation". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2008-02-22. Iliwekwa mnamo Desemba 26, 2007. {{cite web}}: Unknown parameter |deadurl= ignored (|url-status= suggested) (help)CS1 maint: date auto-translated (link)

Kujisomea

[hariri | hariri chanzo]
  • Blinnikov, Mikhail S. A geography of Russia and its neighbors (Guilford Press, 2011)
  • Catchpole, Brian. A map history of Russia (1983)
  • Chew, Allen F. An Atlas of Russian History: Eleven Centuries of Changing Borders (2nd ed. 1967)
  • Gilbert, Martin. Routledge Atlas of Russian History (4th ed. 2007) excerpt and text search
  • Henry, Laura A. Red to green: environmental activism in post-Soviet Russia (2010)
  • Kaiser, Robert J. The Geography of Nationalism in Russia and the USSR (1994).
  • Medvedev, Andrei. Economic Geography of the Russian Federation by (2000)
  • Parker, William Henry. An historical geography of Russia (University of London Press, 1968)
  • Shaw, Denis J.B. Russia in the modern world: A new geography (Blackwell, 1998)

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu: